Mhaga: Kwaresima ya Ukarimu
Njia tano za Kuishi Kwaresima hii kwa Ukarimu
Wapendwa Mahujaji, katika kipindi cha kwaresima, Baba Mtakatifu huwa anatuandikia barua yenye
ujumbe maalum kwa ajili ya mfungo wetu. Umuhimu wa funga yetu unaonekana kabisa
hata kwa kupitia barua hii. Tunaweza, basi kundonoa mambo baadhi ya kutuongoza
katika kuifanya kwaresima yetu iwe karimu kweli.
- Sali zaidi, Funga kwa hiari, na Toa Zaidi
“Kwaresima ni musimu wa
kuzama zaidi katika maisha yetu ya kiroho kwa njia ya kutakatifuzwa inayotolewa
na Kanisa: Kufunga,Kusali na kutoa sadaka.”
Sala, kufunga na kutoa sadaka ni nguzo muhimu katika kukuza imani yetu na
katika kuendeleza ukarimu wetu. Mambo ya kawaida kabisa kama kuacha kula nyama,
tafakari ya kila siku na nafasi ya kutoa/kuwapa wengine vinapewa umuhimu na
KristoYesu mwenyewe (Mt. 6:1-18, 25:31-40). Sali zaidi. Funga kwa hiari yako
mwenyewe. Toa zaidi katika kanisa na kwa maskini jirani zako.
- Jiweke Huru
“Badala ya kuwa chombo
cha kutusaidia kuwatendea mema wengine na kuonyesha mshikamano wetu, fedha
inaweza kutufunga na kutufanya tuishi falsafa ya uchoyo inayoondoa nafasi ya
upendo na kuzuia amani.”
Kwaresima inatupa fursa ya kutafakari vifungo vya maisha yetu vinavyotuweka
mbali na jirani, iwe ni hiyo hela, au mazoeza mabaya au jambo lingine lolote.
Kutoa sadaka na kuwapa maskini ni nafasi mwafaka kabisa ya kutusaidia kufungua
vifungo vyetu na kuwajengea maisha bora wengine waliodhaifu zaidi katika
familia ya watu. Toa sadaka. Wape maskini (Luka 16:19-31). Ubahili, uchoyo, na
uroho ni vifungo hasi katika maisha. Kwa kutoa zaidi, unajiweka huru!
- Neno ni Taa ya Miguu yako
“Neno la Mungu
linatusaidia kufungua macho yetu ili kupokea na kupenda uhai, haswa unapokuwa
dhaifu na legevu. Lakini hili kufanya hivyo, inatubidi kuchukulia kwa uzito
tunachoambiwa na Injili kuhusu yule mtu tajiri.”
Katika parokia yetu, tuna fursa nyingi za majitoleo kila mtu kulingana na
nafasi yake. Na bado, fursa zilizopo za kuzama zaidi katika tafakari ya Neno la
Mungu ni nyingi zaidi. Kila simulizi tunayopata ya maisha yaliyojaa matatizo na
mahangaiko ya ndugu zetu, tunapewa “neno hai” la kutafakari. Tena, kila mtoto
au mtu mzima anayesimulia maisha yake ya ushindi dhidi ya udhaifu na mapungufu
yoyote anatupa sisi “Somo la imani” hai kabisa. Kusoma Neno katika jumuiya na
kushirikishana neno hilo, kuimarishana katika maisha kwa kufarijiana, na zaidi
kuliishi neno hilo ndiyo haswa matendo ya kwaresima. Hija na mafungo, sala za
mtu mmoja mmoja na maungamo, vyote hivi vinatusaidia kuzama zaidi katika kiini
cha kwaresima. Neno ni taa ya miguu yako(Zab. 119:105)!
- Imarisha uhusiano wako na Kristo, Kanisa lake na Jirani yako!
“Kwaresima ni kipindi
mwafaka kabisa cha kupyaisha makutano yetu na Kristo, aliye hai katika Neno,
katika sakramenti na katika jirani zetu.”
Kila kwaresima tunachochewa na kupewa changamoto ya kuimarisha uhusiano
wetu na Kristo, kuja kumjua vyema zaidi—mateso yake, furaha yake na mialiko
yake. Njia mojawapo katika mapokea ya kanisa ni kutembea naye kuelekea Kalvario
katika vituo vya Njia ya Msalaba. Ni kumtangaza Kristo Msulibiwa, wokovu wetu
(1 Kor. 1:23).
Kushiriki kikamilifu katika tafakari ya Njia ya Msalaba ni lishe tosha
kabisa ya nafsi zetu katika kujiandaa kupokea kwa upendo na unyenyekevu zawadi
ya uhai inayopatikana kwa Kifo na Ufufuko wa Bwana. Sala ya Njia ya Msalaba ni
kama utangulizi wa Wiki Kuu na mafumbo yake yote. Shiriki ibada na wengine
uimarishe uhusiano wako na Kristo na kanisa lake. Utaweza kumwona Kristo
mteseka katika maisha ya wengine na kuchochewa kuwaombea wazima na wafu. Mt. Yohane
Paolo II alifundisha: "Yesu Kristo alifundisha kuwa mwanadamu sio tu kwamba hupokea na
kuonja huruma ya Mungu, bali pia anaalikwa kutenda huruma kwa wengine”. Chagua kuvunja miiko yako mwenyewe umwendee jirani yako pawe na upatanisho.
- Shiriki katika Utunzaji wa Mazingira
“Nawahamasisha waamini
waonyeshe upya wa mioyo yao kwa kushirikishana kampeni ya kwaresima inayopangwa
na makanisa sehemu mbalimbali za dunia, na kwa njia hiyo kusaidia katika
kukutanisha watu katika familia moja ya binadamu.”
Ni juu yetu kuona umuhimu wa kutunza mazingira yetu. Maaskofu katoliki
wametoa mwongozo wa Kwaresima ambamo wamesisitiza tuyapende, kuyatunza na
kuyaimarisha mazingira yetu (Ebr. 13:17). Kupanda miti, kutunza bustani zetu na
kusafisha mazingira tunayoishi ni njia mojawapo mwafaka ya kujihakikishia sisi
na ndugu zetu afya ya mwili na roho. Kuweka mazingira yetu safi ni njia ya
kutii agizo la zamani zaidi la kuitiisha nchi (Mw.1:28). Shiriki katika
utunzaji wa mazingira.
Pd. Nicholas Kirimo, SSC
Comments
Post a Comment
Thank you for visiting Bits of the Gospel. We appreciate your comments and support.