Mhaga: Kijiji cha Miujiza
UTANGULIZI
Kwa mgeni anayefika Parokia ya Kisarawe kwa mara ya kwanza, unaweza kufikiria ni parokia yenye mpangilio kama nyingine. Baada ya kugundua kuwa parokia hii ya pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam ina vigango zaidi ya 12, na kwamba kigango cha karibu zaidi kipo kilometa 13 na cha mbali zaidi kilometa 93, hapo utaelewa miundombinu na taratibu hapa ni tofauti na parokia nyingine.
Mwaka huu 2017, Parokia ya Mt. Stefano Shahidi Kisarawe inatimiza miaka 17. Ilizinduliwa mwaka 1999 kuelekea Jubilei ya Mwaka 2000. Katika kuandaa mazingira kwa ajili ya uinjilishaji wa kwanza/msingi, pana umuhimu wa kuanzisha Jumuiya ndogondogo na Vigango. Kila mwaka vijiji ambavyo havina vigango karibu uomba kufunguliwa JNNK. Huo ndio msingi wa vigango vyenyewe.
Jumuiya zinapokomaa na kufunguliwa nyingine, panakuwa na ulazima wa kufungua vigango.
Tuchukue mfano wa Kigango cha Bikira Maria Mama wa Miujiza, Mhaga.
Kwa miaka mingi, ukanda huu wa Pwani hapakuwa kabisa na makanisa katika vijiji vingi. Hata hivyo, baadhi ya wakristo waliohamia katika vijiji vya Wilaya ya Kisarawe walianza kutafuta mahali pa kwenda kusali. Wakristo wa Mhaga walianza kukutana katika nyumba ya Mkristo mmoja na baadaye wakajenga kikanisa cha muda. Hadi mwaka 2016, walikuwa wanasali katika jengo hili la Muda. Lakini jengo hili ni zaidi ya nyumba mbovu. Hapa, mwaka 2013, kanisa lilipokuwa linaadhimisha Mwaka wa Imani, Jimbo Kuu la Dar Es Salaam lilibariki Misalaba na ikatolewa kwa Dekania mbalimbali ili itembezwe na kupelekea wakristo mwamko wa kiimani. Msalaba wa Mwaka wa Imani ulipita hata Kijiji cha Mhaga ambapo ulitua katika kikanisa hiki. Ulifuata mkesha ambao ulivutia wakristo na wasio wakristo.
Wakristo waliripoti miujiza kutokea na kupata faraja na amani ndani ya maisha yao na familia zao. Tunda mojawapo la Msalaba huo kufika hapa Mhaga ni Kanisa Jipya ambalo pia ni Kituo Kidogo cha Hija.
Kanisa la Bikira Maria Mama wa Miujiza ni kanisa la Kigango lakini pia ni kituo kidogo cha Hija. Tarehe 28 Januari 2017, Baba Mhashamu Eusebius Nzigilwa alifika Kijijini Mhaga, kilometa 43 Kutoka Kisarawe Mjini, akiwa katika ziara ya Kichungaji ya Siku Mbili parokiani humo. Na katika ziara hiyo, alibariki kanisa hili kutabaruku Altare yake. Kwa ukubwa, Jengo hili linaweza kuingia watu kati ya 120 hadi 150. Hata hivyo, lilijengwa kwa mtazamo wa kulifanya liwe lenyewe ushuhuda wa Nguvu ya Msalaba. Ni jengo lenye umbo la Msalaba. Mwenyekiti wa Kigango hiki Mwl. Fidelis Chilemba anasimulia:
"Usiku wa Mkesha wa Kupokea Msalaba wa Imani, tulisali tukimwomba Mama Maria atusaidie kupata kanisa la kudumu. Mbele ya Msalaba, tulijinyenyekesha na kuomba kama jumuiya ya waamini. Pamoja na kuombea mahitaji mengine binafsi na ushuhuda tuliopata baadaye wa kuponywa wagonjwa, familia kupata faraja na amani, sisi tunaliona Kanisa hili kama tunda la Msalaba huo. Tunatamani sana kama msalaba huo ungerudi hapa kupamba jengo hili kama ushuhuda wa Kudumu wa Nguvu ya Msalaba."
Baba Mhashamu katika homilia yake alisisitiza kuwa Mahali hapa na jengo hili limeleta uwepo wa Mungu katika kijiji hiki. Mungu amefanya makazi yake kati ya watu. "Mahali hapa pawe nyumba ya kupata faraja na amani katika maisha yenu. Mlitumie jengo hili kuimarisha imani yenu na kuletea kijiji chenu neema kutoka kwa Mungu, alisema."
RAMANI YA JENGO NA MAANA YAKE
Mchoro wa jengo hili na kazi ya kuweka mazingira ya ibada humo ndani kuwa kama yalivyo ni matokeo ya mashauriano kati ya waamini na wachungaji wao. Imani yao na matumaini yao yanaonekana katika jengo hili.
Kwa kuwa Kanisa hili ni juhudi za Wakristo wa Mhaga na msaada kutoka parokia ya Bikira Maria Mama wa Miujiza wa Carnago, Jimbo Kuu la Milano, Italia, mchoro wa Mama Maria, na vioo vyenye Picha ya Mt. Joseph Cottolengo, Bikira wa Miujiza, na Kupashwa Habari Bikira Maria, vyote vimetoka Italia kupitia marafiki zetu huko. Kuna Picha kubwa ya Mama Maria ambayo Marehemu Mario Lanzani alipenda ichorwe na kuwekwa kanisani humo kwa kuenzi Mama Maria.
Hata katika Kupanda Mti wa Kumbukumbu, Baba Askofu alipenda kusisitiza umuhimu wa kutunza mazingira haya yake bustani ya faraja. Nasi tunatamani kwa pamoja kupafanya papendeze pawe kweli Bustani ya Mama Maria. Mauaji wakifika hapa wawe na mazingira matulivu yanayoibua hamu ya kusali na kupumzisha mwili.
RATIBA NA MATUKIO YA MWEZI MACHI
Tarehe 13 Machi 2017, waamini wa Vigango cha Masaki, Kisanga, Sungwi & Kisanga, wataenda kuhiji huko Mhaga wakiomba wapate Parokia Mpya kwao. Kanisa wanalo lakini wanahitaji Nyumba ya Mapadre.
Tarehe 25 Machi 2017, waamini kutoka Kigango cha Mzenga watakutana huko na Waamini kutoka Parokiani katika hija na adhimisho la Sherehe ya Kupashwa habari Bikira Maria kuwa Mama wa Mkombozi.
NENO LA ZIADA
Kigango cha Mhaga kina Jumuiya tatu: Jumuiya ya Bikira Maria Imakulata, Jumuiya ya Bikira Maria Mfariji, na Jumuiya ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi.
Kama kituo kidogo cha Hija, wanahitaji mabechi ya Kanisa, Viti, kuweka uzio eneo la Kanisa n.k.
Comments
Post a Comment
Thank you for visiting Bits of the Gospel. We appreciate your comments and support.