Mhaga: Lolote atakalowaambieni, Fanyeni!

Lolote atakalowaambieni, fanyeni! (2:1-12)
Utangulizi
Biblia ni barua ya Mungu. Kwa kuisoma tunamjua, tunaungana naye na kujipatia mwanga wa maisha yetu. Aidha, tunapata hisia chanya takatifu: tunahisi kupendwa, kusamehewa na kusaidiwa naye. Tukisoma na kulitafakari neno kwa makini tunatambua kuwa jambo alilomfanyia mwafulani/Israeli katika Biblia Mungu yu tayari kutufanyia kama hilo.
Yesu, Maria na Kanisa Lake
Katika harusi ya Kana ya Galilaya—Mama Maria yupo. Lakini na Yesu na wanafunzi wake walialikwa. Hapo, ishara ya kwanza itatendeka kwa ombezi la Mama Maria. Lakini tujiulize maswali matatu:
a)      Mbona wanaharusi watindikiwe divai? Ina maana gani?



b)      Mbona ni Maria tu anayetambua hilo hitaji? Bila kuombwa tena.
c)      Bila Yesu na Maria ingekuwaje harusi ya Kana?
Maria ni Jicho la Mungu
Kwanza, kulingana na mapokea Maria alijiimarisha sana katika upendo wa jirani. Labda umaarifu wake unatokana na kuwa Mama wa “Mwalimu Yesu”. Lakini mbona “Msema Chochote” haoni hitaji—alipaswa kuliona kwa sababu ni jukumu lake—lakini Maria asiyehusika ndiye anayeliona? Tuone kwamba Maria hakualikwa, lakini alikuwepo! Kadiri ya Zaburi 139, Mungu anajua maisha (yakiwemo mahitaji, mapungufu) yetu hata kabla ya kutuumba. Moyo wa Maria “uliliona hitaji” la Elizabeti (mama wa Yohane Mbatizaji) bila kuitwa au kualikwa, akaenda kumhudumia kwa miezi mitatu. Kifupi nafikiri kuwa Maria ni jicho la Mungu, la kuonea mahitaji yetu hata yale tusipokwalika au kumwomba.
Mungu aliyeyaona mateso ya Waisraeli waliokuwa utumwani Misri (Kut. 3:7). Sasa anamtumia Maria kama jicho lake la kuonea mahitaji ya watu! Lakini tuelewe kwamba moyo wa Maria wenye hisi ya Mungu ndilo jicho la Mungu.
Maria anakuwa kiungo, njia, daraja kati ya Mungu (Yesu) na wanaharusi (waamini wote). Ndio maana Maria anaonana kutoa mwelekeo, agizo kwa wahudumu: “Fanyeni lolote atakalowaambia” (Yoh. 2:5). Katika haya ya 7, Yesu anawaagiza, “Jalizeni mabalasi haya maji”. Waliyajaza furi. Yalikuwa sita. Agizo la pili, “Choteni mmpelekee mkuu wa meza.” Kumbe maji yalishageuka kuwa divai—tena bora kuliko ile iliyotengenezwa na maharusi!
Fadhila ya Utii
Hilo limetendeka kwa sababu wahudumu wametii agizo la Yesu! Petro na wenzake walivua bila kuambulia chochote (Luka 5:4). Tupa jarife katika kina cha ziwa na utapata: walipata samaki 153!
Kutindikiwa divai kwa wanaharusi kunakuwa uwanja wa kutendea muujiza! Ina maana Mungu alipotuumba tuna vikomo, dhambi ya asili, madhaifu na juu ya yote kutindikiwa wokovu, aliandaa jukwaa la kututendea miujiza. Na kama Musa alishika nafasi ya mshenga mkuu—Yesu amejitwalia Ushenga Pekee!
Lakini Mt. Joseph Cottolengo alifasiri nafasi ya Maria katika mpango wa wokovu: “Baada ya Yesu yupo Maria Mtakatifu!” Yaani, Maria ni mshiriki mkubwa zaidi wa wokovu wangu na wa wote. Anajua dunia nzima inahitaji nini—hasa sala, wongovu na amani. Hata tukio la Mwaka huu la kuadhimisha miaka 100 tangu Maria kutokea watoto wa Fatima, ujumbe wa Mama Maria ni uleule. Sala, wongovu na amani.
Nipo katika Historia ya Wokovu
Maria ananijua na anakujua. Anajua tunachotindikiwa. Hiyo ndiyo divai yako. Kama divai ni kileta furaha katika harusi, wewe nawe unachotindikiwa ni kileta furaha katika maisha yako.
Lakini agizo la Maria, “fanyeni kila atakalowaambieni”, kutimizwa kwa agizo hilo kulileta muujiza.
Mungu humwambia kila mmoja wetu:
a)      Tubu na uiamini injili (Yesu) -
b)      Omba na utapewa, bisha hodi utafunguliwa, tafuta utaona -
c)      Unapenda kunifuata? Jikane mwenyewe, chukua msalaba wako kila siku, nifuate -
Tunajua kuwa Mungu alimwagiza baba yetu na mama yetu, Adamu na Eva wakakaidi—wakajipotezea na kutupotezea wokovu. Sasa Maria ndiye Eva mpya. Anatufundisha kwa maisha, uamuzi na utekelezaji wake jinsi ya Mungu kufanya muujiza mkuu kuliko yote: kumruhusu Mungu kugeuka kuwa mwanadamu (na bado anabaki kuwa Mungu).
Tufanye nini?
Tushike agizo lake Maria. Fanyeni lolote atakalowaambia.

Tunaweza kutimiza mambo kadhaa aliyotuagiza Yesu:
yohane 15:7... “Ukiungana nami na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo na mtafanyiwa. Hila lina maana: Kukaa katika hali ya neema na kuomba chochote!
Njia rahisi kabisa za kuungana na Mngu ni kusali bila kuruka muda wa sala uliojipangia. Sala iwe nyofu, ya imani, tumaini na upendo kwa Mungu. Kumwomba Mungu kupitia Bikira Maria. Yesu hawezi kumkatalia Maria mamaye lolote amwombalo kwa niaba yetu na kwa ajili yetu. Kuungana na Mungu kwa Imani. Wahebrania 11:6, neno linasema hatuwezi kumkaribia Mungu wala kumpendeza Mungu—hivyo safisha imani yako. Ondoa dhambi yako, kujiamini kuliko Mungu, ndumba, ushirikina.... Halafu mtumainie Mungu kwa uwezo wako wote kana kwambahuwezi kujitendea chochote. Hizi fadhila  za Kumungu imani, tumaini, upendo zinatuunganisha na Mungu.

Pd. Philip Ntonja, SSC
15 Machi 2017
Mhaga

Comments

Popular posts from this blog

TYCS - Muungano wa Mt. Cottolengo (MOCK)

Mwana Mpotevu au Waana Wapotevu?