Mwana Mpotevu au Waana Wapotevu?
Injili ya Kwaresima:
Utangulizi
Nafikiri sio rahisi sana kutoa tafakari kuhusu Mwana Mpotevu. Inaitwa pia
Injili ya Baba mwenye huruma. Tutagundua kuwa ina majina zaidi ya haya leo. Mojawapo
ya vipengele vinavyovutia zaidi vya Maisha ya Kiroho (mafundisho) ya Mt.
Joseph Cottolengo ni msisitizo anaweka katika “Kuwa katika uhusiano mwema na
Mungu”. Alitaka ziive kati ya wafuasi wake na Mungu. Na Injili hii (Luka
15:11-32) inatusaidia kutathmini kama tupo sawa. Labda inafaa kufikiria ni wana wawili wapotevu. Hebu tuitafakari pamoja kama Walezi wa Watoto Wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu.
Kupotelewa na Mwana!
Huzuni. Niaminini kweli. Unaweza kuvumilia mara mia kupotelewa na kondoo
au hata hela (haya 1-10) kuliko kuvumilia kupotelewa na mtoto. Injili hii
utumika mara nyingi kama maandalizi ya maungamo. Inaonyesha picha ya Baba
asiyekata tamaa, mwenye huruma kubwa. Hisia tunazopata kuhusiana na tabia ya
huyu kijana aliyepotea, na kule kurudi kwake kwa baba, kunaibua maswali
lukuki.
Hivi, ule ubavu wa huyu mjinga kumwendea baba na kudai kutaka mgao
wake/sehemu yake unavumilika na mzazi kweli? Sio hilo tu, yale majivuno
(akatwaa vyote akaenda mbali ugenini... 13) yanavumilika kweli? Kuharibu mali
yote katika maisha ya anasa ni ujinga. Lakini ni ujinga zaidi kutaka kurudi
nyumbani baada ya kumaliza mali. Ila kwa baba, mwanae amepotea. Hajali mali
alizotapanya. Baba hana majuto. Hana hasira. Anatamani mwanaye harudi. Kama
anatafuta taarifa, anataka kujua kama yupo hai, kama ana afya. Kama anapeleka
salamu, anamtakia mwanae mema, anamwalika harudi. Kila siku anasimama
mlangoni na kuangalia kwa subira. Matumaini, huruma, subira... ndizo fadhila zake.
Kurudi kwa Mwana Mpotevu
“Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu... (18). Maamuzi. Mateso
yanamfanya mwana akumbuke upendo/ukarimu/wema wa baba yake. Unamtamanisha
maisha aliyoacha. Anaamua kurudi. Kurudi kwake ni ishara ya kutubu. Tayari
ametubu, amejutia dhambi zake. Hata kama hajui baba atampokea vipi, badala ya
kumwogopa baba, anaamua kwenda kwake. Anajiandaa kuungama dhambi zake.
Anafanya orodha ya makosa yake.
Kurudi kwake kunaibua sherehe. Kanzu, viatu, ndama aliyenona... ishara za
kupokelewa upya, za kurudishiwa hadhi yake/heshima/nafasi yake katika
familia. Na Pete? Pete ni ishara ya kuinuliwa zaidi kiheshima. Ni alama ya
wazi ya upendeleo wa baba. Kama kanzu tayari ni ishara ya upendeleo (kumbuka
Yusufu mwana wa Yakobo?), pete inaonyesha ameinuliwa juu zaidi. Muziki,
kucheza, kula na kunywa... karamu kubwa. Baba anaadhimisha kurudi kwa mwanae!
Kurudi kwa Mtoto wa Kwanza
Mzaliwa wake wa kwanza anarudi, anaikaribia nyumba, anasikia vifijo na
ngoma. Kwa taarifa yenu, mwanzo wa sura hii, tumeambiwa kuwa watoza ushuru
wote na wakosefu walimjia wapate kumsikia. Mafarisayo wakalalamika wakisema,
huwapokea wakosefu na anakula nao. Hivyo hii karamu hii ya kumpoka mdhambi
aliyerudi inafanana na karamu anazoshiriki Yesu akiwapokea wadhambi
waliorudi. Na kumbe wakati watu wakiwa wanakula ndipo Yesu aliwakatisha
akaanza kusimulia story hii. Nawaona watu walivyokaa kimya wakimsikiliza.
Naona hamu yao ya kusikia ujumbe huu mpya.
Turudi kwa mwanae wa kwanza/mkubwa. Anapopata habari kuwa sherehe hiyo ni
kwa ajili ya mdogo wake, ananuna. Aha? Kuna nini? Ni sherehe asiyotarajia.
Baba anamwendea. Kama mwanae mdogo alimjia (alimrudia) hapa baba anaenda
kumsihi huyu aingie ndani washerehekee. Hebu oneni ilivyo, huyu anakataa
kusherehekea kwa sababu anahisi baba hatendi haki. Je, sio hivyo kwetu pia?
Sisi nasi hatutamani kuona baba akitenda haki. Namaanisha, amwadhibu mwanae
kidogo. Amwonyeshe alichofanya sio sahihi? Aiya! Kurudi hivi hivi ni rahisi
akaamua kwenda tena!
Wewe ni nani katika story
hii?
Ni rahisi kujiona kama mwana mpotevu. Wakati mwingine kila mmoja wetu
anakuwa mwana mpotevu.Nanatamani “kuwa huru”—kutembea anapopenda, kutumia
mali ovyo, kujiachia! Kwa nadra sana nakuwa kama baba. Nionyeshe huruma bila
kutamani kuadhibu, kukashifu, kukosoa, kueleza? Labda. Lakini bado
haijatokea. Inakuwa vigumu kujiona kama mtoto wa kwanza. Huyu anajitokeza
zaidi katika maisha yetu. Tunatamani watu waovu wapate adhabu “hili
wajirudi”. Kwetu, njia ya msamaha haina uhakika wa kumfanya mkosefu hajirudi
kama njia ya adhabu na ukali. Je, unajisikiaje unaposikia hukumu ikitolewa
kwa kibaka, mwizi, mhuni? Tunasema haki itendeke!
Oneni jinsi tulivyo wagumu wa kuiga baba yetu? Kweli sisi ni wanae?
Tunafanana naye? Nina mashaka sana. Oneni tunavyotamani tutendewe vyema zaidi
ya waovu heti kwa sababu tumemtumikia Mungu? Waovu wakipata mema, tunajisikia
vibaya. Wakati Neno la Mungu linatuonyesha wazi kuwa mvua yake uwanyeshea
wema na waovu sawa. Wakati Yesu ameliongelea tena siku aliposimulia kuhusu
wale watu waliokwenda shambani, asubuhi, mchana, jioni na wote wakaripwa
denari moja. Kilio cha wale wa kwanza kilikuwa, “Tumefanya kazi zaidi ya hawa
waliokuja kazini jioni saa kumi na moja. Tunastahili kutendewa vyema zaidi.”
Mbele ya Mungu tunaweza kudai haki kweli? Oneni tulivyo wapendwa!
Hitimisho
Tuvae viatu vya mtoto wa kwanza tuone alivyojikuta katika hali ngumu
kumwelewa baba yake. Ni kwaresima. Msishangae. Ni kwaresima wakati
tunaposafisha maghala yetu. Mimi nipo bize kufanya usafi kwangu. Sina taimu
ya kuangalia kama wengine wapo safi au la. Naamini wapo safi kuliko mimi.
Aha! Na kama walezi, tusaidianeni kuwa wema bila kuoneana vivu, bila
kujifikiria kuwa wa pekee sana. Tukikumbana na ugumu,
tujikumbushie/tukumbushane kuwa sisi ni watoto wa kwanza. Tunatii sheria tu.
Upendo wa dhati kwa baba sio mazoea yetu. Hila tunajua kuwa Mungu anatupenda.
Hatukati tamaa.
SALA
Ee Mungu mwenyezi, tunakushukuru. Kwaresima ni kipindi cha neema ndani ya
mwaka wa kanisa. Ahasante kwa kipindi hiki. Halafu, wewe unayewapenda wanao
wote, yule aliyepotelea mbali na huyu aliyepotelea nyumbani, tusaidie na sisi
kupendana na kuhurumiana kama wewe unavyotuhurumia. Tupe neema ya kuwa
wavumilivu kama wewe ulivyo mvumilivu. Tuwezeshe kuwa karibu na wadhambi hili
nao waonje upendo wako. Amina!
|
“...Mt. Joseph Cottolengo ni msisitizo anaweka katika “Kuwa katika uhusiano
mwema na Mungu”.
“...Kanzu, viatu, ndama aliyenona... ishara za kupokelewa upya, za kurudishiwa
hadhi yake/
heshima/ nafasi yake katika familia..”
“...Nionyeshe huruma bila kutamani kuadhibu, kukashifu, kukosoa, kueleza?
Labda. Lakini bado haijatokea..”
Ahsante sana kwa ujumbe mzuri na wenye kuleta tumaini hasa katika kipindi hiki cha Kwaresma. Ubarikiwe!
ReplyDelete