Palm Sunday 2011

Dominika ya Matawi – Siku ya Vijana Ulimwenguni
Tumsifu Yesu Kristu! Mapendo! ….
Mt. 26:14-27:66 Wahusika na majina yao ya mitaani
Baadhi ya watu tunaokutana nao katika injili ya leo ni maarufu kiasi cha kuwa na nickname.
1. Yuda Iskariote
Yuda hana jina la mtaani kwani jina lake tayari ni matusi. Linatosha.
Ni mmoja wa wale thenashara, wale marafiki kumi na wawili wa Yesu. Marafiki? Utamwitaje Yuda rafiki? Mnafiki labda inafaa.
Uhusiano wake Yuda na Yesu ni fumbo kweli. Alikuwa mmoja wa wafuasi wake wa karibu. Hakuwa katika lile kundi kubwa lililomfuata Bwana kwa mbali, mara kwa mara, au katika matukio makubwa. Yaani, Yuda hakuwa mmoja wa wale wakristu wanaojitokesha kipindi cha Kwaresima, Mkesha wa Pasaka/Krismasi, au siku kama ya leo ya matawi. Alikuwepo kila siku. Ni mmoja wa wale wanaosali ibada za kila asubuhi, alishiriki mipango yote ya jumuiya ya wafuasi wa Yesu. Yuda, kama mimi na wewe alikuwa karibu na Yesu, katika Mwili lakini sio Mtazamo! Ninapoongea kuhusu Yuda, napenda sana kumtetea. Napenda nikutane naye, nimkumbatie na kumnong’oneza: “Tupo pamoja, kaka. Mwanangu, nilichukia kwamba watu wanakusema lakini sikujua nifanye mimi. Yote waliyosema kuhusu wewe, yalinigusa kama vile waliyasema kuhusu mimi”.
Yuda, aliaminiwa na Yesu sana. Aliaminiwa na wanafunzi wengine. Kumbukeni alikuwa mhazini wa kundi hili. Mimi niliyeaminishwa makubwa na Mungu nanyi ndugu zangu; wewe uliyepewa nafasi ya uongozi au heshima katika kundi. Tujifikirie sana. Wanaoaminiwa ndio mwisho wa siku wanaokosa kuwa waaminifu. Usiingie katika majadiliano na adui wa Kristu kwani wao wanajua udhaifu wako. Bali, ongea na marafiki wa Kristu kwani wao wanajua nguvu zako.
Yuda, alipogundua kosa lake alijinyonga! Pole sana. Mimi nataka kuishi. Nataka nipate nafasi ya Kuambia Yesu kwamba Nampenda. Mpaka hapo, hisia zako Yuda na zangu, mtazamo wangu na wako viliwiana. Lakini kwa hili la kutotubu, mimi naona kuna sababu na hitaji la kutubu.
MWISHO WA TAKAFAKARI YA YUDA ISKARIOTE.
2. Petro
Jina la mtaani la Petro ni coward. Yeye ni mwoga sana. Kama wahenga walivyonena, “Mbwa abwekaye sana, hang’ati.”
Msikie. “Hata kama watu wote watakuwa na mashaka nawe, mimi sitakuacha kamwe.” [33] Hivi hamwafahamu watu wa aina hii? Mimi nitamwambia waziwazi. Msihofu, nikiwepo mambo yote sawa. Halafu mbaunsa akijitokesha wa kwanza kutoweka....
Hila, Petro ni mtu mwenye nia njema. Anaogopa macho na maneno ya binti mmoja mdogo, wanawake wawili, na umati. Anaishia kumkana Yesu. “Mimi, Simjui mtu huyo!” [70, 72, 74]. Mara tatu. Halafu. Jogoo anawika. Hapo sasa.
Jogoo anayewika kila wakati ninapotenda maovu ni dhamiri yangu. Inanisuta. Sina jinsi. Lazima niisikie. Kama Petro, ni mara nyingi natoka kwenda kuangua kilio, cha kimya kimya. Kweli lazima iwe hivyo. Lazima niende kuungama. TAFAKARI YA PETRO INAENDELEA KILA SIKU.
3. Pilato, Kuhani Mkuu, na Jemedari/Maaskari
Hawa wahusika wa tabia zinazofanana. Ni watu wenye mamlaka na wanaofuata sheria. Hawajui zaidi ya kutii sheria na kuzitekeleza. Pilato, kwa kumhoji Yesu anauliza, “Wewe ndiwe mfalme wa wayahudi?” Nina mashaka na ujuzi wa kazi wa Pilato. Hivi, wenzangu katika Imani, swali lifaalo zaidi lisingekuwa, “Wewe ni nani?” Lakini, Pilato anajua Yesu ni nani. Kwa hivyo jibu la Yesu kwake ni sahihi, “Wewe umesema.” [27:11] Halafu anaendelea, “Mwataka nimfungue nani, Baraba au Yesu aitwaje Kristu.” Basi, kumbe anajua kabisa kwamba ni Kristu, yaani mpakwa-mafuka wa Bwana, Masiha. Anajua. Hataki kuamini kwa sababu atapoteza nafasi yake machoni pa watu. Hivi, haijatokea kwako kuhairisha mabadiliko, kutubu... huku ukijisemea moyoni, “Wataoniona au kusikia kwamba nilikuwa naungama watanifikiria nini?” Heshima yangu itashuka!!
Halafu, Kuhani Mkuu, kama Pilato anajua Yesu ni nani. “Tuambie kama wewe ndiwe Kristu, Mwana wa Mungu.” [63] Hapo sasa. Kumbe sio mpakwa mafuta tu, bali ni Mwana wa Mungu! Kuhani Mkuu anajua. Lakini kama mtu aliyelewa anayeongea kiingereza, hajui analojua. Wewe je, unajua unalojua. Yaani, unayoyatamka katika Nasadiki, unayaelewa kweli. Ama tunatamka maneno tu, wenzangu. Nawaombeni tujue kutafakari angalau mara kwa mara, yote tunayoyatamka katika sala. Isiwe kwetu kama kwa kuhani Mkuu, [halafu ni kuhani!], “Wewe umesema!”
Maaskari hawana jipya, ndugu zangu. Hawana jipya kabisa. Wao, kama kawaida, wameamrishwa na katika kutekeleza wajibu wao, wamekumbana na haya ya leo. Ni dhahiri kwamba wanawasikia watu wakisema kwamba ni mwana wa Mungu. Lakini, katika kumtesa hawakurifikiria. Hatuongei kuhusu maaskari waliopo. Naongea kuhusu watu wengi walioketi humu ambao wanapenda kutekeleza kajukumu/amri bila kutafakari. Mwisho wa siku, wanakuwa wamesimama mbele ya Mungu huku wakilalamika kwamba Mungu amewatelekeza! “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Ni hitimisho, wanafikiria. Wanaona kwamba “alikuwa” mwana wa Mungu. KUNDI HILI TUSILISAHAU. TAFAKARI YAO INAENDELEA.
Mwisho...
Ndugu waamini, hatuna budi kujiuliza maswali kadhaa. Hivi, ni mara ngapi tunakuwa kama hawa watu tuliosikia katika simulizi la leo? Ni mara ngapi tunakuwa katika umati tukiimba “hosana” na dakika chache baadaye, yule yule tuliyekuwa tunaimbia, “Tusaidie-hosana” tunasema, “Asulibiwe!”? Nauliza, ni mara ngapi tunakuwa kama wale wayahudi wanafiki na wenye fitina, wasiokubali kushindwa. Hata baada ya Kumwua Yesu, wanaendelea bado kumbatiza: hamjasikia walivyosema, “Yule Mjanja alisema... [Mt. 27:63].
Asiyetaka kufanya maamuzi ya kumwamini Kristu, yaani ya kubadilika na kuanza maisha mapya, atasema, Yule mjanja na wajanja wenzake alisema tubadilike kwa maslahi yake/yao. Kama vipi? Mimi nataka kumfuata hata kama ni mjanja. Alisema atafufuka na kweli hata baada ya kulinda kaburi, alifufuka kwa sababu Ufufuko wake sio swala la mazingaombwe. Kuweka ulinzi ni swala la kitoto. Katika Ufufuko ni Mungu anayetekeleza mpango wake. Mpango wake, kwa taarifa zenu, auzuiliki.
Mapendo!

Comments

Post a Comment

Thank you for visiting Bits of the Gospel. We appreciate your comments and support.

Popular posts from this blog

TYCS - Muungano wa Mt. Cottolengo (MOCK)

Mwana Mpotevu au Waana Wapotevu?