KONGAMANO LA VIJANA, MWAKA WA IMANI (PAROKIA YA KISARAWE)
KONGAMANO: OVERLAND HIGH SCHOOL, MARUMBO
UTANGULIZI
"Someni kwa bidii, jiwekeni daima karibu na Mungu, na mkuze fadhila za uchapakazi na uadilifu kuanzia umri huu mdogo. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwenu." Maneno hayo ya Mhashamu Askofu Titus Joseph Mdoe, ni nasaha iliyoliashiria kufikia kilele cha Kongamano la Vijana, Mwaka wa Imani lililoandaliwa na Ofisi ya Vijana, Parokia ya Kisarawe.
Kuanzia tarehe 06/06/2013, Alhamisi Jioni hadi 09/06/2013 Jumapili Jioni, takriban vijana 180 walishiriki pamoja na walezi wao katika lililochukua kaulimbiu yake kutoka Injili ya Luka.
Luka 17:5 "Bwana Tuongezee imani”.
Katika kufanikisha lengo la Kongamano hili, walezi wa Vijana wakiongozwa na Pd. Kirimo walihamasisha na kusimamia maandalizi yaliyochukua zaidi ya mwezi mzima. Mada Kadha wa kadha zilitolewa ikiwemo Kujikuza katika Imani (Nd. Silvanus M.), Utunzaji na uwekezaji katika Mazingira (Mwelimishaji Mkuu kuhusu Mazingira, Kanda ya Pwani), Uchumba na Ndoa (Nd. Pascal Maziku), Mafundisho ya Kanisa kuhusiana na Utoaji Mimba (Dr. Sr. Msimamizi wa Cardinal Rugambwa Hospital), Imani Potovu za Ushirikina, Uchawi na Nguvu za Giza (Pd. Kirimo). Sr. Hellen na Sr. Maria Cesalia waliongea kuhusu mada za Miito na maisha ya Sala katika nyakati tofauti tofauti. Palikuwa na Mdahalo kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya na Ushiriki wa Vijana ulioongozwa na Nd. Mathias Kazonda, maarufu kama MC Paleari, ambaye ndiye makamu mwenyekiti Parokia.
Sambamba na mada hizi, vijana walikuwa wameandaa nyimbo, mashairi, maigizo, vichekesho na mengine kuendana na mada hizi. Palikuwa pia na fursa za kubadilishana mawazo kati ya vijana waliotokea vigango 6 kati ya 10 vya parokia ya Kisarawe. Walishiriki wawakilishi wa parokia ya Vingunguti na viongozi wa TYCS wa Kanda ya Mt. Aloyce, Pugu.
Wakati Kongamano hili likiendelea, wazo la kutafuta mbinu za kuwaunganisha zaidi vijana hawa liliibuka. Ni katika juhudi hizo palipopatikana kundi la sanaa la pamoja lililoandaa maigizo ya siku ya Kilele, Mechi za kirafiki kati ya Vigango na Parokiani, na ile kwaya iliyoimba katika Misa ya Kufunga Kongamano.
"Bidii na Uadilifu"
Baada ya nasaha za viongozi mbalimbali, Mhashamu Askofu Titus Joseph Mdoe alionekana mchangamfu kabisa alipowapongeza viongozi na walezi wa vijana kwa wazo kama hili la kupeleka huduma karibu na waamini. Kongamano hili ni la kwanza kufanyika katika maeneo ya Kigango. Makongamano na Matamasha yaliyopita yalifanyika parokiani. Kigango cha Maneromango ambapo inapatikana Shule ya Overland kipo takriban kilometa 62 kutoka Kisarawe Mjini, lilipo Kanisa la Parokia.
Katika juhudi za kutafuta uzima, watu mbalimbali ujishughulisha na mambo yanayowapa uzima wa kimwili na kiroho. Akinukuu Injili ya siku husika, Askofu Mdoe aliwasisitiza vijana kupenda sana kuchapa kazi bila kujihurumia kwani uvivu (ambao ni mwiko!) unazaa rushwa, wizi, na maovu mengine mengi. Katika Mwaka wa Imani, mafundisho yaliyotolewa yanapaswa kudumu katika maisha ya vijana kama msukumo wa ndani wa kuwawezesha kuishi imani yao ipasavyo.
"Kanisa linawategemea vijana kama mojawapo ya makundi muhimu zaidi. Vijana wanaashiria uhai wa kanisa. Hivyo, vijana mkishika Imani na kuiishi kikamilifu, mnapata uhai. Mnapata Uzima. Ndio uzima aliouleta Kristo kwetu," Askofu alisema.
Kuandikwa Historia
Ujio wa Mhashamu Askofu Mdoe umeweka historia. Ndio mara ya kwanza kabisa kwa askofu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam kufika maeneo ya vigango vyetu. Kutokana na umbali na ubovu wa barabara, haikuweza kufikirika kwamba askofu angeweza kufika katika Vigango vyetu!" Paroko alisema. "Nathubutu kusema leo historia imeandikwa upya kwetu sisi!"
Mheshimiwa Sila, Mmiliki na Meneja wa Shule ya Overland alionekana mwenye furaha isiyo na kifani aliposimama kulihutubia Kongamano hilo. "Sijui tulichaguliwa kwa kigezo kipi. Nashukuru sana kwa upendeleo huu. Mlezi anasema kuwa ukarimu wetu umewapatia nafasi ya kuandika historia. Mimi sijui. Nashukuru sana."
Sherehe ya Kufunga Kongamano ilifanyika kwa kuchangisha kwa ajili ya mfuko wa Kongamano. Walioweza kutoka walijieleza kuwa wamehamasika vilivyo. Wengine waliahidi kutoa chochote kidogo baadaye.
Hitimisho
"Ushirikiano kati ya Ofisi ya Vijana, Parokia na Ofisi ya Vijana, Jimbo utatusaidia kuwaleta pamoja vijana wengi zaidi. Tunakuomba Baba Mhashamu utusaidie katika hili." Vijana walisema katika risala yao. Askofu aliwahakikishia kwamba ushirikiano huo utaboreshwa chini ya uongozi wake. Pia Mhashamu alipenda kuwaondolea wote hofu kwamba vijijini ni mbali. Alieleza kwamba yupo tayari kabisa kufika hata mbali zaidi ilimradi wakristu wapate huduma hii.
Basi kati Kata ya Marumbo, wilaya wa Kisarawe, historia iliandikwa pale ambapo Roho Mtakatifu alisimamisa na kuongoza kundi la walezi, vijana, na Uongozi wa Shule ya Overland kuratibu maandalizi ya Kongamano hili. Baba Askofu Titus Mdoe akaweka saini yake katika kitabu cha kumbukumbu. Ikumbukwe basi, Vijana -- Mapendo daima!
Comments
Post a Comment
Thank you for visiting Bits of the Gospel. We appreciate your comments and support.