Tutafakari Maisha yake
Hand drawing-St. J B Cottolengo by Kirimo |
Ni dhahiri kabisa kwamba Mt. Joseph Benedict Cottolengo sio tu mwana wa Mungu bali mwana Mpendwa na Mpenda Mungu. Upendo huu wa pekee kwa Mungu ulitokana na imani yake dhabiti. Kama Kijana alielimika katika mafundisho makuu ya imani. Alijua kuwa Mungu ametupa wote upendeleo wa pekee sana, ambapo kila mmoja wetu alipewa nafasi ya pekee machoni pa Mungu.
Kwanza kabisa, imani hii ilimjengea msimamo na tabia ya aina yake. Katika utendaji kazi wake kama padre, alijitahidi kuwa na upendo wa pekee kwa kila mmoja, akiwapa nafasi ya kwanza maskini na wanyonge. Ni upendo huu ambao ulimsukuma (Caritas Christi) kumwishia Mungu katika Maskini wa kila aina. Picha ya Mt. Cottolengo kama padre inakuwa kamili tunapomfikiria kama baba--Baba wa maskini. Kumbe Mt. Cottolengo alikuwa akimuiga Mungu Baba katika upendo wake kwa watu wote. Tena Mt. Cottolengo alikuwa akimleta Kristo na upendo-okovu (Saving love) katika maisha ya wanyonge ambao kiurahisi wanajiona kama wasiofaa.
Pili, Mt. Cottolengo, sio tu kwamba alivutiwa na upendo usio-na-masharti wa Mungu Baba Mpaji, bali alikubali kuwa "Mfanyakazi wake asiye na taaluma". Katika kujieleza, yeye alijua vizuri nafasi yake. "Mmiliki (na meneja) wa Chumba Kidogo cha Mungu Mpaji ni Mungu Mwenyewe! Mimi ni mfanyakazi asiye na taaluma, alipendelea kusema." Kimsingi alichokubali ni "kuvaa" tabia za kimungu ili maskini waone uso wa Mungu Baba Mpaji ndani yake. Kwa walioishi pamoja na Mt. Cottolengo, waliona na kushuhudia kwamba upendo wake ulikuwa wa Kibiblia. Alijitahidi kugawa mkate kwa wote, kuponya magonjwa ya moyoni kwa kuwafariji walio mahututi... kuwa msafirimwenza wa wote waliokuwa katika njia ya mateso (Via Doloris).
Tatu, mtakatifu mwanzilishi wetu alipenda kweli kwa sababu alitambua naye kwamba alikuwa amependwa kweli. Malimwengu yasingemvutia na kummeza kama yanavyoonekana kuwavuta na kuwafunga wengi siku zetu. Kwake yeye, upendo wa kweli haukuwa nadharia bali maisha halisi ya kila siku. Alionja kila siku upendo huu usio na mipaka. Alivyoufungulia upendo huu, uligeuka kuwa kama mto naye akawa bomba la kupitia upendo huu. Maskini waliweza kukiri kuwa Mt. Cottolengo alikuwa "Chombo cha neema, upendo na uwepo wa Mungu".
Tuombe nasi, wapendwa. Hili pamoja na Mt. Cottolengo, Mwenyeheri Paleari, Msifiwa Bruda Luigi Bordino, na wafuasi wengine wengi wa njia hii ya kiroho, tushiriki tabia hii ya kimungu, ya kupenda bila masharti. Tuombe hili juhudi tunazofanya kujenga maisha haya zituletee neema na kugeuka kuwa kichocheo cha kutafuta utakatifu.
Mt. Joseph Benedict Cottolengo, Utuombee!
Comments
Post a Comment
Thank you for visiting Bits of the Gospel. We appreciate your comments and support.