Kanda ya Mt. Aloyce, Pugu: Tawi la Kimani


Ufunguzi wa Tawi la Kimani Secondary School – Kisarawe

Kanda ya Mt. Aloyce – Pugu                           Friday, May 10, 2013

_____________________________________________________

Utangulizi

Kwa mkusanyiko huu wa watu, kwa maandalizi haya ya kipekee kabisa, kwa Ibada hii ya Misa Takatifu, tunazindua rasmi tawi la TYCS Kimani, Kanda ya Mt. Aloyce Pugu. Ni tendo la imani. Na kwetu vijana wakatoliki, ikizingatiwa kuwa huu ni Mwaka wa Imani, sina shaka kabisa tendo hili linatuimarisha zaidi kiroho. Kama TYCS ni chama cha Kitume kinachowaleta pamoja Vijana Wakatoliki wa Shule za sekondari hili kumleta Kristo katika mazingira ya shule, ni wazi kabisa kwamba leo, kwa njia ya Pekee, Kristo anakuja katika mazingira ya shule ya Kimani (Wilaya ya Kisarawe).

Yesu anakuja sio kuingilia programu za shule au kuvuruga amani yetu kama wanafunzi bali kutuimarisha katika shughuli nyeti iliyotuleta hapa Kimani Sekondari. Ni katika kufuata maadili na mafundisho ya kijana mkatoliki unapogeuka kuwa mdau imara wa shule hii.

Tafakari

Tupo katika Novena ya Roho Mtakatifu, Siku tisa za mwishoni za kipindi cha Pasaka. Ni katika siku hizi tunasubiria Roho Mtakatifu. Paulo mtume anatukumbushia kuwa, kama Kristu asingefufuliwa, kuamini kwetu, majitoleo yetu … hata hii shughuli ya ufunguzi wa tawi, ni bure (Taz. 1 Kor 15:17). Na bila zawadi hii ya Kristo Mfufuka, hatuna la kijivunia!

Mtume Paolo ni mfano mzuri tu wa jinsi imani katika Kristo inavyoweza kumbadilisha mwanadamu—uovu wa mwanadamu daima hauwezi kushinda wema wa Mungu. Mwuuaji aligeuka kuwa mlinzi mkubwa wa uhai. Mpinga Kristu akawa mhubiri wa Injili ya Kristo. Labda kuna mmoja wetu anayejidhania kuwa kashindikana? Labda yupo mmoja wetu anayejifikiria kwamba amekuwa mbaya sana kiasi cha kufanana na shetani mwenyewe? Paulo analetwa kwako leo ujione na wewe kama mmoja wa walioitwa kukumbatia injili hiyo hiyo uliyokuwa ukipinga kwa maisha yako yasiyo na maadili, yasiyo na msimamo, yasio na Mungu! Alitesa wengine! (Kutesa… maana ya kiswahili sanifu), sasa yeye anateswa. Alipinga, sasa anapingwa. Alidhulumu sasa anadhulumiwa. Sio kwa sababu malipo ni papa hapa! Bali kwa sababu  Yesu aliye (a) Nuru Yoh 8:12, limwangazia; (b) Neno la Uzima Yoh 6:68 alisema naye, (c) Ufufuko , alimfufua kutoka kifo cha dhambi, Yoh 11:25.

Na leo Yesu anatuambia tena, “Ninyi mtalia na kuomboleza bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha (Yoh 16:20). Maneno haya anayasema kwetu sote: kila mwanadamu anayetamani kuishi upendo kwa Mungu na Jirani, hata kama akiri imani yake katika Kristo, yeye ni mfuasi wa Kristo. Kwa kutaka kutafuta haki na amani, atapingwa. Kwa kutaka kusimamia ukweli na usawa, atapata adui wengi. Watu watakuwekea kila aina ya mtego ili uanguke, ujikwae, uumie, ukate tamaa au hata ufe. Kwa sababu, Mwanadamu anapotafuta yaliyo mema, anafanana na Mungu. Mwanadamu anapojitwika msalaba wake na wa wengine kuhakikisha kuwa anajenga ujirani mwema—usiojua dini, itikadi, mwegemeo wa chama, elimu, jinsia na ujinsia, rangi na tofauti nyingine zozote zile, huyo anafanana zaidi na Kristu Yesu! Atapingwa na kutafutiwa kila aina ya mitego kama Yesu, Mwana wa Mungu alivyojikuta akipingwa na wengi.

Hitimisho

Katika mateso yote hayo, Sali. Endeleza urafiki wako wa siri na Mungu. Waache waseme. Wana haki ya kusema na kufikiria kama wanavyopenda. Una haki ya kuwa sababu ya maongezi yao. Sio kwa maovu unayosambaza bali kwa mbegu za wema unazopanda kila kukicha.
 Leo F. Buscaglia alisema: Usifikirie kuwa ukitumia muda wako kujiuliza kwa nini maisha yanaonekana kuwa katika hili duni hivi, unafanya la maana. Hapa, unapoteza muda tu. Badala yake, jiulize, nifanye nini niboreshe maisha haya? Hapo utapata jibu. Kila siku na mzigo wake! 

Ni vyema kila mmoja wetu akafiria hivi: Nipo hapa kujenga maisha yangu ya leo na ya kesho. Maisha yangu yakiwa na mwelekeo chanya, wengine watanufaika. Hiyo ndiyo furaha ambayo ulimwengu hauwezi kuwaondolea.

 

Comments

Post a Comment

Thank you for visiting Bits of the Gospel. We appreciate your comments and support.

Popular posts from this blog

TYCS - Muungano wa Mt. Cottolengo (MOCK)

Mwana Mpotevu au Waana Wapotevu?